Jumanne, 20 Januari 2015

Saratani ya tezi dume si ugonjwa mpya, ni muuaji wa kimyakimya!





 Dar es Salaam--Watu wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kujua ugonjwa wa saratani ya tezi dume, huku wakidhani ni mpya. Lakini ukweli ni kuwa umekuwapo miaka mingi na wengi wameugua.

Takwimu zinaonyesha wanaume wengi huugua ugonjwa huu unaoongezeka kwa kasi ya hali ya juu.
Kulingana na utafiti uliofanywa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORIC), kutoka mwaka 2006, zinaonyesha kuwa kila mwaka kumekuwa na ongezeko la kesi mpya ya wagonjwa saratani ya tezi dume.

Novemba ya kila mwaka, jumuiya za kimataifa huadhimisha tukio ambalo hujulikana kama Movemba.
Maadhimisho hayo huhusisha kukuza kwa masharubu, kukusanya fedha na kuleta mwamko na ufahamu wa masuala ya afya kwa wanaume kama vile saratani ya tezi dume.

Jina hilo la Movemba ni mchanganyiko wa neno ‘Masharubu na Novemba’.
Maadhimisho hayo ya mwezi mzima yanalenga kuongeza ufahamu na mwamko kwa kupima ili kugundua mapema.

Mwaka jana peke yake zaidi ya Dola za Marekani 120 milioni zilikusanywa.
Hadi sasa, Movemba imekusanya zaidi ya Dola 550 milioni kupitia wanachama wake milioni nne katika nchi 21 duniani kote.

Waziri mstaafu wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa alinukuliwa akisema asilimia 10 ya wagonjwa wanaosumbuliwa na aina mbalimbali za saratani wamejitokeza hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.

Anasema asilimia 90 iliyobaki hawajafanya jitihada zozote kuhudhuria uchunguzi na matibabu.
Akizungumzia juu ya uchunguzi wa hali ya tezi dume nchini, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Hospitali ya Apollo yenye makao makuu India, Dk Prathap Reddy anasema kuwa ugonjwa huo unaathiri watu wengi na kusababisha vifo vingi nchini kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu wa kina juu ya ugonjwa huo.

Utaratibu wa uchunguzi wa saratani ya tezi dume haufanyiki kutokana na gharama na ukosefu vifaa vya uchunguzi nchini.

''Watu wengi hurejea hospitali wakati ugonjwa huo upo katika hatua ya mwisho na hauwezi kuzuilika tena. Hata hivyo, kuna uwezekano wa ugonjwa huo kutibika endapo utagundulika mapema.''

Pamoja na kuwapo kifaa maalumu cha utambuzi wa saratani ya tezi dume ‘chaprostate specific antigen’ (PSA) duniani, Watanzania wachache wana uwezo wa kupata huduma hii.

Kwa sababu kifaa hiki kina gharama kubwa na kinahitaji wafanyakazi wenye ujuzi na upimaji wenyewe ni gharama kubwa.

Mchungaji Dk Emmanuel Kandusi aliyenusurika na saratani ya tezi dume ana uzoefu wa kutosha juu ya ugonjwa huu na anajaribu kujenga ufahamu na uelewa kwa wananchi wenzake.
Tofauti na Watanzania wengi Dk Kandusi alikuwa na uwezo wa kupata matibabu ushauri kutoka nje ya nchi.
Wakati akiugua alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Apollo.
“Kutokana na maendeleo na upatikanaji wa vifaa muhimu na wafanyakazi wa kutosha katika hospital hiyo nilikuwa na uwezo wa kuokoa maisha yangu na kuanza kuwaelimisha wengine,” anasema.

Ukilinganisha mazingira yaliyoko katika hospitali za nje ya nchi kama Apollo na hali ya taasisi zetu za afya hakuna uwiano. Hadi sasa nchi ina kituo kimoja tu tiba ya mionzi ya saratani yaani ORCI.
 Mahitaji ya wagonjwa wa saratani nchini haishabihiani na huduma zenyewe.

Kutokana na tatizo hili na ukweli kwamba ORCI hakiwezi kukidhi mahitaji yote ya wagonjwa wote wa aina mbalimbali za saratani, mathalani wagonjwa hulazimika kwenda kupata matibabu yao India hususani kwenye Hospitali za Apollo.

Saratani ya tezi dume ni aina ya saratani ambayo huanzia kwenye tezi za kibofu ya jinsia ya kiume itokanayo na ukuaji hafifu wa seli inayopelekea uvimbe katika tezi.

Baada ya hapo seli za saratani husambaa kutoka kwenye tezi dume kwenda sehemu nyingine za mwili hususan katika mifupa na matezi ambayo husababisha maumivu hasa katika kupitisha haja ndogo na wakati wa tendo la ndoa.

Hii ni aina ya saratani ambayo hushambulia zaidi wanaume walio juu ya miaka 50.
Tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonyesha kuwa wanaume walio chini ya miaka 40 wana uwezo wa kupata saratani ya tezi dume kwa uwiano wa mtu mmoja kati ya 100,000.

Kwa wanaume walio kati ya miaka 70 na 74 wako katika hatari ya kupata saratani hiyo kwa wastani wa watu 1,326 kati ya 100,000.

Hali kadhalika inakisiwa mwanamume mmoja kati ya sita hupata saratani ya tezi dume katika maisha yao .
Kila mwaka kati ya wanaume wote wanaogundulika na saratani moja ya nne wana saratani ya tezi dume.
Desmond Tutu anasema ugonjwa huu wa saratani ya tezi dume kuwa hauna mipaka ya kijamii.

Dalili
Dalili za tezi dume ni matatizo katika mfumo wa haja ndogo pamoja na kwenda haja mara kwa mara hususan usiku na kushindwa kuistahimili kwa muda.

Nyingine ni matone ya damu kati haja ndogo, maumivu katika sehemu ya chini ya mgongo, upotevu wa hamu ya kula na kupungua uzito.
Ili kugundua saratani ya tezi dume, mgonjwa anahitaji uchunguzi wa kina katika njia yake ya haja ndogo ambako daktari hujaribu kuhisi uvimbe wowote utakao kuwa katika mfumo wa mkojo na matezi uchunguzi ambao hufuatiwa na vipimo vya damu

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni