Jumapili, 25 Januari 2015

Kutembea kwa dakika 20 kila siku, huongeza siku za kuishi



Dar es Salaam--Kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mtindo wa maisha umebadilika ikiwamo watu wengi kutumia usafiri wa magari hata kwa safari ya umbali mfupi.

Mabadiliko hayo ya maendeleo kwa kiasi kikubwa yamekuwa chanzo cha watu wengi kuwa wavivu wa kufanya mazoezi hata yale rahisi, kiasi cha kusababisha mwili kutokuwa mwepesi.

''Kutembea ni mojawapo ya mazoezi yasiyokuwa na masharti makubwa na magumu ambayo kila mmoja anaweza kufanya kwa nafasi yake''

Jambo la kushukuru na kufurahia ni kile kilichoelezwa na watafiti wa tawi la Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Marekani kuwa kutembea kwa dakika 20 kila siku huongeza muda wa kuishi kwa asilimia 16 hadi 30.

Wataalamu hao walisema kuwa, kutembea kwa muda huo kila siku hupunguza hatari ya kupata maradhi kama shinikizo la damu, saratani, kisukari.

Waliendelea kueleza kuwa kutembea kwa dakika 20, kwenye umri wa ujana husaidia kupunguza gharama za matibabu wakati wa uzeeni.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Phoenix, umebainisha kuwa kutembea kwa dakika 20 huongeza umri wa kuishi na kupunguza gharama za matibabu.

Wataalamu wa chuo hicho walikusanya washiriki 20,667 wa umri kati ya miaka 40 na 79 , miongoni kila siku walitembea kwa dakika 20 na wengine hawakupewa zoezi hilo.

Walibaini waliokuwa wanafanya zoezi hilo wanaishi kwa kutumia gharama kidogo zaidi ya wale wasiofanya.

Walibaini kuwa kati ya watu waliofanya zoezi hilo kulikuwa na waliokuwa na tatizo la kisukari na shinikizo la damu, huku baadhi yao wakiwa wameanza kupoteza kumbukumbu lakini baada ya kufanya mazoezi hayo mfululizo walipona au kupunguza hatari ya kufariki kwa maradhi hayo.
Wataalamu hao walirahisisha zaidi kwa kusema kuwa hata wale ambao hawakutembea dakika zote 20, mara moja bali waligawa mara tatu kwa siku walipata faida pia.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), watu wengi zaidi katika maeneo yote duniani wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa kuharusi, moyo na saratani kutokana na kutokufanya mazoezi.

Takwimu za WHO zinaonyesha maradhi kama shinikizo la damu na unene wa kupita kiasi vinaongezeka kutokana na watu kushindwa kufanya mazoezi.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni