Jumatatu, 2 Februari 2015

Acha kula chumvi nyingi kuepuka maradhi ya moyo









Dar es Salaam--Inakadiriwa pia kuwa ifikapo mwaka 2020 magojwa ya kuambukiza yatakuwa na uwiano sawa na magonjwa yasiyoambukiza. Hii inatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama maradhi ya moyo kuongezeka miaka hadi miaka.

Moja ya mambo ambayo yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa matatizo ya moyo ni ulaji wa chumvi. Chumvi ni moja ya kiungo kinachoweka ladha katika vyakula.


''Chumvi ni muhimu pia mwilini. Huusaidia mfumo wa fahamu katika kutekeleza kazi zake, kujivuta kwa misuli, udhibiti wa kiwango sahihi cha maji na uwiano sahihi wa chumchumvi mwilini''


Chumvi hutumika pia kwa ajili ya kudhibiti wingi wa maji katika damu, ogani na tishu za mwilini. Pale chumvi inapozidi basi figo huwa na kazi ya kuitoa kwa njia ya mkojo.

Chumvi ikiwa nyingi figo hushindwa kutoa kiasi chote na kubakia mwilini hivyo kusababisha matatizo.

Watu wengi hula chumvi nyingi na hujikuta wakiongeza wanapopatiwa chakula. Wengi hawafahamu kama ulaji chumvi kwa mtindo huu ni hatari kwa afya zao.

Msukumo wa damu mwilini hutegemea na uwepo chumvi na pale inapozidi mwilini msukumo wa damu nao unakuwa juu. Hali huwa mbaya kwa yule ambaye tayari ana matatizo ya moyo. Watu ambao kwao kuna historia ya shinikizo la damu ni vizuri kuchunga na kupunguza matumizi ya chumvi katika chakula.
Chumvi nyingi husababisha magonjwa mengine kama vile kiaharusi. Hii hutokea pale msukumo wa damu unapokuwa mkubwa zaidi na kusababisha mishipa ya damu kuathirika.

Mishipa ya artery huweza kuharibika na kuwa myembamba au kusinyaa na kuta zake hukukaamaa. Hali hii huufanya moyo kuwa na kazi ngumu na hivyo inakuweka katika hatari ya kupata shambulizi la moyo la ghafla, moyo kushindwa kufanya kazi au kiharusi.

Matatizo mengine ni kama vile moyo kuwa mkubwa na valvu kuwa na matatizo. Hii inatokana na ujazo mkubwa katika mzunguko wa damu, hivyo kuufanya moyo uwe na kazi ya ziada ili kuwa na mzunguko sahihi unaotakiwa na mwili.

Kadiri muda unavyosonga na uwepo wa hali hii husababisha moyo kuongezeka ukubwa na valvu za moyo huwa nyembamba. Hali hii husababishamaumivu ya kifua, kushindwa kupumua na kuwa na uchovu usioisha. Pia kifo cha ghafla na moyo kushindwa kufanya kazi huweza kutokea.

Chumvi pia husababisha magonjwa mengine kama ya figo, mwili kuvimba na upungufu wa maji, tindi kali kuwa nyingi tumboni na udhaifu wa mifupa.

Namna ya kutumia chumi ipo kanuni ya dole gumba. Kiasi unachofinya ndicho kinatakiwa kiwepo kwenye kila mlo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni